17 Oktoba 2022 - 19:39
Rais Raisi: Marekani imehusika katika vitendo vya kikanda vya hujuma, mauaji na ghasia

Rais Ebrahim Raisi wa Iran amelaani vikali uungaji mkono wa Marekani kwa machafuko ya hivi karibuni nchini Iran, akisema mikono ya Marekani inaonekana wazi katika vitendo vingi vya hujuma, mauaji na ghasia katika eneo.

Akihutubia kikao cha baraza la mawaziri Jumapili mjini Tehran, Rais Raisi amesema: "Matamshi [ya hivi karibuni] ya Rais wa Marekani [Joe Biden], ambaye anajiruhusu kuchochea moto wa machafuko, mauaji na uharibifu katika nchi nyingine, yanatukumbusha maneno ya kudumu milele ya mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu [Ayatullah Ruhullah Khomeini] ambaye aliitaja Marekani kuwa 'Shetani Mkuu”.

Rais wa Iran ametoa kauli hiyo ikiwa ni katika kujibu matamshi ya hivi punde ya Biden ambaye alidai kuwa "ameshangazwa" na jinsi Wairani walivyotoa radiamali kufuatia kifo cha Mahsa Amini aliyekuwa na umri wa miaka 22, ambaye alianguka katika kituo cha polisi na baadaye kufariki hospitalini. Rais wa Marekani amedia kuwa anasimama na taifa la Iran kikamilifu.

Baadhi ya raia wa Iran wamefanya maandamano kufuatia kifo cha Amini. Hata hivyo, baadhi ya watu wenye itikadi kali walivuruga maandamano hayo na kuchochea ghasia dhidi ya vikosi vya usalama. Vyombo vya habari vinavyoungwa mkono na nchi za Magharibi pia vimechochea  ghasia.  Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasema haitaruhusu kuingiliwa masuala yake ya ndani.

Kwingineko katika matamshi yake, Rais wa Iran amesema: "Sababu za msingi za hujuma, mauaji na machafuko mengi katika eneo zikichunguzwa, nafasi na uovu wa Marekani unaweza kugundulika kwa urahisi."

Waibua ghasia wanaopata himaya ya Marekani wakiwa wameteketeza mali za umma nchini Iran

Hali kadhalika Rais Ebrahim Rais amesema, "Takriban miaka 70 ya uungaji mkono kwa uhalifu [unaofanywa na] utawala wa Kizayuni huko Palestina na pia miongo miwili ya uvamizi na uchochezi wa Wamarekani nchini Afghanistan ni mifano ya hatua za Shetani Mkuu."

Amebainisha kuwa, "Marekani inachukizwa na hatua yoyote nzuri, ya kiubunifu ya taifa la Iran na kufurahishwa na mapungufu au matatizo ya Wairani pamoja na ukosefu wa usalama."

Raisi amesisitiza kuwa,"Taifa lenye ufahamu la Iran linamfahamu vyema adui na hila zake na wakati huu [kwa mara nyingine tena] litamzuia adui kufikia malengo yake na litaendelea kwenye njia ya ustawi na maendeleo,"

342/